Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Vicky Kamata
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Vicky Kamata,anatarajiwa kugawa vitabu 5,000 vya masomo ya Sayansi, Kiingereza na Hesabu kwa shule mbalimbali za Kata za Mkoa wa Geita kwa lengo la kuendeleza elimu.
Akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki, Kamata alisema mkoa huo una zaidi ya shule za kata 100 na baadhi yake zitanufaika na vitabu hivyo vya masomo ya ziada.
“Vitabu hivyo nitavigawa katika shule za kata za mkoa mpya wa Geita ambao unakabiliwa na changamoto nyingi kama vifaa vya kufundishia, maabara na mabweni kwa kuanzia nimeanza na vitabu 5,000 nilivyovipata kwa juhudi zangu,” alisema.
Alisema kupitia nafasi yake ya ubunge, ataendelea kuipigia serikali kelele ili shule hizo zipate vifaa mbalimbali vinavyohitajika ili kuboresha elimu mkoani humo.
Aidha, alisema mbali na kugawa vitabu hivyo, pia atagawa vyandarua, mablanketi na baiskeli kwa watu wenye ulemavu ambazo amezipata kupitia marafiki wa taasisi yake ya Victoria.