Mkurugenzi Mtendaji Wa Global Education Link, Mr Abdulmalik S. Mollel akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
Global sasa yamaliza kilio cha Wazazi wanaosomesha Watoto Nje Ya Nchi.
ASILIMIA 99 ya wazazi wanaosomesha watoto wao vyuo vya nje ya nchi wamekuwa wakishindwa kulipia ada ya masomo yao kwa mkupuo, kutokana na hali ya kiuchumi ikilinganishwa na ada kuwa kubwa katika vyuo hivyo.
Hayo yalisemwa jana Novemba 3,2013 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link Mr Abdulmalik S. Mollel wakati wa uzinduzi wa Mikopo ya Wanafunzi wanaosoma Vyuo Vya Nje ya Nchi, kwa kushirikiana na Benki ya Afrika(BOA Bank).
Mollel amesema kuwa baada ya kusikia kilio cha wazazi hao
ikilinganishwa na hali ya kiuchumi kuwa sio nzuri kwa baadhi ya Watanzania huku
wananfunzi wakiwa na nia nzuri na vigezo vya kuendelea na masomo lakini gharama
kubwa zinawafanya kukosa fursa hizo za kusoma nje ya nchi.
“Unajua sisi kama Global tumesikia kilio cha Wazazi hao
ambao wana nia ya kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi lakini kutokana na
masharti ni lazima mzazi alipe fedha hizo za ada kwa wakati mmoja jambo ambalo
limewawia vigumu kulipa kwa wakati mmoja kwahiyo tukaona tuanzishe programu hii
ya kuwakopesha ili waweze kufikia malengo yao na ndoto za watoto wao,”alisema
Mollel.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya kozi ambazo hazipatikani hapa
nchini badala yake zinapatikana nje ya nchi huku gharama zake zikionekana kuwa
kubwa na kuwashinda wazazi ingawa wanakuwa na nia ya kuwapatia watoto wao elimu ya kozi
hizo lakini wanashindwa.
Baadhi ya kozi hizo ni pamoja na uhandisi wa mafuta,kozi za
ndege yaani rubani,upasuaji wa ubongo na kozi nyingine ambazo hazitolewi nchini
Tanzania na kwamba kwa sasa kilio hicho kinakaribia kuisha kama sio kupungua
kutokana na mikakati ya Kampuni ya Global kuhusu elimu ya vyuo vya nje ya nchi.
Amewaomba wazazi wote ambao wana wanafunzi wenye vigezo vya
kuweza kuomba nafasi za vyuo vya nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kwani suala
la kushindwa kulipa ada sio tatizo tena.
Serikali imeyataka makampuni kuiga
mfano wa Global.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi Ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bw.Zuberi M.Samataba, akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
SERIKALI imeyataka mashirika na makampuni binafsi kuiga
mfano wa Kampuni ya Global Education Link Limited katika kusaidia masuala
mbalimbali likiwemo suala la elimu ili kuipunguzia serikali mzigo wa kufanya kila
jambo.
Hayo yalisemwa jana Jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu Ofisi Waziri Mkuu
Tamisemi Zuberi Samataba wakati wa uzinduzi wa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma
vyuo vya nje ya nchi na kwamba kitendo cha Kampuni hiyo kwa kushirikiana na
Benki ya Afrika (BOA) ni kitendo cha kuigwa na baadhi ya makampuni, mashirika na
Taasisi binafsi katika kuinua elimu nchini.
“Kusema ukweli kampuni hii ni mfano wa kuigwa katika suala
la kuwawezesha Watanzania kupata elimu nje ya nchi maana hata mimi ni shahidi
mwanangu wa kwanza anayesoma nje ya nchi alisaidiwa na Global kwahiyo kitendo
hiki kinatufanya kushirikiana kwa ukaribu zaidi kuhakikisha kampuni hii
inaendelea kuwawezesha Watanzania kupata elimu nje ya nchi,”alisema Samataba.
Samataba alisema kuwa kuna watoto wengi wenye uwezo mzuri
kimasoma lakini uwezo wa kupata elimu ya juu limekuwa tatizo kubwa na
ikilinganishwa na upatikanaji wa baadhi ya kozi hapa nchini sio kozi zote
zinapatikana hapa jambo ambalo linamlazimu mzazi kumtafutia mwanaye kozi hizo
nje ya nchi lakini gharama zake zinakuwa juu na kumfanya ashindwe kutimiza
ndoto zake.
Samataba amesema kuwa baada ya kuzindua mpango huo wazazi
wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanajisajili ili kuweza kuwapatia watoto wao
elimu nje ya nchi zikiwemo kozi ambazo hazipatikani ndani ya nchi.
TCU yawatahadharisha Watanzania juu
ya kupata vyuo bora nje ya nchi
Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU), Profesa Magishi Nkwabi Mgasa,akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
TUME ya vyuo vikuu Tanzania (TCU),imewatahadharisha
Watanzania kuwa makini wanapotafuta nafasi za masomo katika vyuo vya nje ya
nchi badala yake wakapate ushauri katika Tume hiyo pamoja na mawakala wa vyuo
hivyo waliopo Tanzania.
Hayo yalisemwa Novemba 3, 2013 Jijini Dar es salaam na Kaimu Katibu
Mtendaji wa TCU Profesa Magishi Nkwabi wakati wa uzinduzi wa Programu ya mikopo kwa
wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya nje ya nchi iliyozinduliwa Novemba 3, 2013.
Programu hiyo inafadhiliwa na Kampuni ya Global Education
Link Limited chini ya Mkurugenzi wake Abdulmalik Mollel ambapo wanafunzi
wanaosoma nje ya nchi wataweza kukopeshwa baada ya kupata chuo na kutimiza
vigezo.
Nkwabi alisema kuwa kuna baadhi ya vyuo nje ya nchi
havitambuliki hapa nchini baada ya mwanafunzi kumaliza masomo yake katika chuo ambacho hakitambuliwi na TCU ni kama vile mwanafunzi amepoteza muda wake bure na
kwamba kwa sasa kutokana na jitihada za kampuni ya Global suala la udanganyifu
litaweza kuisha.
“Napenda kuwaambia wazazi pamoja na wanafunzi kuweni makini
maana kuna baadhi ya vyuo nje ya nchi havitambuliwi na TCU,kwahiyo tayari kuna
fursa hii ya Global itumieni ili waweze kuwaelekeza na kuwasaidi namna ya
kupata vyuo vilivyo bora na kutambuliwa na TCU,”alisema Profesa Nkwabi.
Alisema kuwa Global ni kampuni ambayo wamekuwa wakifanya
kazi kwa ukaribu sana na kupewa ushauri katika masuala ya vyuo vya nje ya nchi
na kwamba kwa sasa kampuni hiyo inaonekana kufanya vizuri na sasa imeleta mpango
ambao ni ukombozi kwa Watanzania na kuwaomba kutumia fursa hii kutimiza ndoto
zao katika elimu.
Wizara ya Elimu yaipongeza Global
Mkurugenzi Wa Elimu Ya Juu, Wizara Ya Elimu Na Mafunzo Ya Ufundi, Profesa Sylivia S. Temu,akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
WIZARA ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi imeipongeza Kampuni ya Global Education Link Limited kutokana
na mpango wake wa kuanzisha mpango wa kuwapatia mikopo wanafunzi wanaosoma vyuo
vya nje ya nchi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu
Profesa Sylivia Temu wakati akizindua programu hiyo Novemba 3, 2013 Jijini Dar es salaam
na kwamba serikali haina budi kuwapongeza hasa katika suala la elimu kwa kutoa
mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi.
“Napenda kuipongeza Kampuni ya Global kwa niaba ya Wizara ya
elimu, maana hili ni suala kubwa sana la kuwakopesha wanafunzi wanaosoma nje ya
nchi ni kitendo cha kuigwa na makampuni mengine hapa nchini maana elimu ndiyo
kila kitu kuna baadhi ya wazazi wanapenda kuwasomesha watoto wao nje ya nchi
lakini hali ya uchumi hairuhusu pamoja na kuwa na vigezo, hongereni sana,”alisema
ProfesaTemu.
Aliahidi kutoa ushirikiano kwa kampuni ya Global ili mpango
huo usiishie hewani badala yake uwe mkombozi kwa Watanzania wote wenye nia ya
kupata elimu nje ya nchi na kwamba Taifa lenye watu wasomi ndilo
linaliofanikiwa kiuchumi na katika mambo mengine.
Aliwaomba Wananchi kutumia fursa hii kwa wenye vigezo kupata
mikopo ili kuweza kupata elimu nje ya nchi hasa kwa kozi ambazo hazipatikani
hapa nchini na kuweza kuzipata katika vyuo hivyo vinavyotoa kozi hizo.