SAID JUMA IRANDO2
Dar es Salaam. Mwanafunzi bora wa kwanza kitaifa katika matokeo
yaliyorekebishwa ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2012,
Said Irando kutoka Shule ya Sekondari Feza ya jijini Dar es Salaam,
ameeleza kushangazwa na matokeo hayo kwa kuwa hakuyatarajia.
Mwanafunzi huyo ambaye tayari ameshaanza masomo ya
Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Feza, alisema kuwa ingawa
alisoma kwa bidii lakini hakudhani kama angeweza kushika nafasi ya
kwanza kitaifa na kwamba anamini mafanikio yake kitaaluma yana ‘mkono wa
Mungu’.
“Sikutegemea kabisa kuwa mwanafunzi bora, ingawa
nilisoma kwa bidii kubwa nia yangu ilikuwa ni kutaka kufaulu tu; Ni
Mungu amenisaidia,” alisema Irando.
Alisema kujituma katika masomo, mazingira mazuri
ya kusomea na upatikanaji wa vifaa muhimu vya kujifunzia ndiyo
yaliyomwezesha kusoma na kufanya vizuri.
Irando ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia
yenye watoto watatu, alisema kurekebishwa kwa matokeo ya kidato cha nne
kulibadilisha alama za matokeo yake kutoka Daraja la kwanza akiwa na
alama tisa hadi saba, zilizomfanya kuwa mwanafunzi bora kitaifa na
mwafunzi bora wa kwanza kati ya wavulana kumi bora pia kitaifa.
Mwanafunzi huyo alibainisha kuwa pamoja na wazazi
wake kuwa ni wafanyabiashara, yeye anatamani kuwa mhandisi ingawa bado
hajajua atakuwa mhandisi katika tasnia gani.
“Natamani sana kuwa mhandisi hiyo ndiyo ndoto yangu ingawa bado sijajua nitakuwa mhandisi wa sekta gani,” alisema Irando.
Irando alisoma elimu ya msingi katika Shule ya
Msingi J.K Nyerere ambako alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Sekondari
Pugu, lakini wazazi wake waliamua kumpeleka Shule ya Sekondari Feza.
Naye mwanafunzi Joshua Azza kutoka Sekondari ya
Wavulana Marian ambaye ameshika nafasi ya saba kitaifa kati ya wanafunzi
kumi bora baada ya kupata daraja la kwanza akiwa na alama 11, alisema
ameyapokea matokeo hayo kwa furaha akiamini atatimiza lengo lake la kuwa
daktari wa upasuaji.
“Natarajia kuwa daktari wa upasuaji, kwa matokeo
haya nadhani nitafanikiwa,” alisema Azza ambaye wazazi wake wote ni
walimu alipozungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Saidi Nchimbi kutoka Sekondari ya
Feza, ambaye ameshika nafasi ya nane kati ya wanafunzi kumi bora
kitaifa, alisema kuwa siku zote alikuwa akisoma kwa uwezo wake wote na
kwamba alikuwa akitamani kufaulu kwenye mitihani yake yote aliyopewa.
Nchimbi amefanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya
kupata daraja la kwanza akiwa na alama nane. Katika matokeo ya awali
mwanafunzi huyo alikuwa na alama 11.