Mkurugenzi Mtendaji Wa Global Education Link, Mr Abdulmalik S. Mollel akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
Global sasa yamaliza kilio cha Wazazi wanaosomesha Watoto Nje Ya Nchi.
ASILIMIA 99 ya wazazi wanaosomesha watoto wao vyuo vya nje ya nchi wamekuwa wakishindwa kulipia ada ya masomo yao kwa mkupuo, kutokana na hali ya kiuchumi ikilinganishwa na ada kuwa kubwa katika vyuo hivyo.
Hayo yalisemwa jana Novemba 3,2013 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link Mr Abdulmalik S. Mollel wakati wa uzinduzi wa Mikopo ya Wanafunzi wanaosoma Vyuo Vya Nje ya Nchi, kwa kushirikiana na Benki ya Afrika(BOA Bank).
Mollel amesema kuwa baada ya kusikia kilio cha wazazi hao
ikilinganishwa na hali ya kiuchumi kuwa sio nzuri kwa baadhi ya Watanzania huku
wananfunzi wakiwa na nia nzuri na vigezo vya kuendelea na masomo lakini gharama
kubwa zinawafanya kukosa fursa hizo za kusoma nje ya nchi.
“Unajua sisi kama Global tumesikia kilio cha Wazazi hao
ambao wana nia ya kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi lakini kutokana na
masharti ni lazima mzazi alipe fedha hizo za ada kwa wakati mmoja jambo ambalo
limewawia vigumu kulipa kwa wakati mmoja kwahiyo tukaona tuanzishe programu hii
ya kuwakopesha ili waweze kufikia malengo yao na ndoto za watoto wao,”alisema
Mollel.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya kozi ambazo hazipatikani hapa
nchini badala yake zinapatikana nje ya nchi huku gharama zake zikionekana kuwa
kubwa na kuwashinda wazazi ingawa wanakuwa na nia ya kuwapatia watoto wao elimu ya kozi
hizo lakini wanashindwa.
Baadhi ya kozi hizo ni pamoja na uhandisi wa mafuta,kozi za
ndege yaani rubani,upasuaji wa ubongo na kozi nyingine ambazo hazitolewi nchini
Tanzania na kwamba kwa sasa kilio hicho kinakaribia kuisha kama sio kupungua
kutokana na mikakati ya Kampuni ya Global kuhusu elimu ya vyuo vya nje ya nchi.
Amewaomba wazazi wote ambao wana wanafunzi wenye vigezo vya
kuweza kuomba nafasi za vyuo vya nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kwani suala
la kushindwa kulipa ada sio tatizo tena.
Serikali imeyataka makampuni kuiga
mfano wa Global.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi Ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bw.Zuberi M.Samataba, akihutubia wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mikopo Kwa Wanaosoma Vyuo Vya Nje Ya Nchi.
SERIKALI imeyataka mashirika na makampuni binafsi kuiga
mfano wa Kampuni ya Global Education Link Limited katika kusaidia masuala
mbalimbali likiwemo suala la elimu ili kuipunguzia serikali mzigo wa kufanya kila
jambo.
Hayo yalisemwa jana Jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu Ofisi Waziri Mkuu
Tamisemi Zuberi Samataba wakati wa uzinduzi wa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma
vyuo vya nje ya nchi na kwamba kitendo cha Kampuni hiyo kwa kushirikiana na
Benki ya Afrika (BOA) ni kitendo cha kuigwa na baadhi ya makampuni, mashirika na
Taasisi binafsi katika kuinua elimu nchini.
“Kusema ukweli kampuni hii ni mfano wa kuigwa katika suala
la kuwawezesha Watanzania kupata elimu nje ya nchi maana hata mimi ni shahidi
mwanangu wa kwanza anayesoma nje ya nchi alisaidiwa na Global kwahiyo kitendo
hiki kinatufanya kushirikiana kwa ukaribu zaidi kuhakikisha kampuni hii
inaendelea kuwawezesha Watanzania kupata elimu nje ya nchi,”alisema Samataba.
Samataba alisema kuwa kuna watoto wengi wenye uwezo mzuri
kimasoma lakini uwezo wa kupata elimu ya juu limekuwa tatizo kubwa na
ikilinganishwa na upatikanaji wa baadhi ya kozi hapa nchini sio kozi zote
zinapatikana hapa jambo ambalo linamlazimu mzazi kumtafutia mwanaye kozi hizo
nje ya nchi lakini gharama zake zinakuwa juu na kumfanya ashindwe kutimiza
ndoto zake.
Samataba amesema kuwa baada ya kuzindua mpango huo wazazi
wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanajisajili ili kuweza kuwapatia watoto wao
elimu nje ya nchi zikiwemo kozi ambazo hazipatikani ndani ya nchi.