“Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni, wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe la Kagame inapokelewa bungeni. Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au viwanjani…” alisema.
Alisema wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka walikuwa ni wengi na walichangia kwa kiasi kikubwa matokeo kuwa mabaya.
Dk Ndalichako alionyesha baadhi ya michoro hiyo ambayo inaonyesha vikaragosi ambavyo wanafunzi hao waliviita Messi (Lionel, mchezaji wa Barcelona) na zombi (ni picha za kutisha) ambazo huonyeshwa kwenye televisheni.
Sababu za kufeli
Dk Ndalichako alisema hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja juu ya kwa nini matokeo ya mwaka huu yamekuwa mabaya, lakini akadokeza kuwa huenda yametokana na wanafunzi wengi kukosa maarifa.
Anasema mbali na waliojaza matusi na michoro, wanafunzi wengine waliofanya vibaya ni wale ambao hawakujaza chochote kwenye karatasi zao za majibu.
“Kuna baadhi ya shule unakuta darasa zima watoto hawajajibu somo fulani kwa mfano Biolojia, wanaingia tu na kuandika namba. Tuliamua kuwapigia simu walimu wao, majibu waliyokuwa wakitupa ni kuwa hawajawahi kuwa na walimu wa somo husika kwa hiyo watoto hawakuwa na cha kujaza.”
Dk Ndalichako alisema kwa ku mbukumbu zake, hakuna matokeo mabaya kama ilivyo kwa mwaka huu yaliyowahi kutokea.
“Tukiangalia tu kuanzia 2000, hakujawahi kutokea matokeo mabaya kama haya, kwa kweli hali haipendezi. Hata kabla ya kuyatangaza nilikuwa nayaangalia mara tatu tatu, sikuyapenda na inasikitisha kwa kweli,” alisema Dk Ndalichako.