Jumla ya wanafunzi 3,821 waliokuwa na sifa ya kupata mikopo
katika elimu ya juu, hawakupata mikopo hiyo na hivyo kushindwa kuendelea
na masomo yao, Bunge lilielezwa jana.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo aitoa kauli hiyo jana alipokuwa akijibu maswali bungeni.
Alisema wanafunzi waliokosa mikopo ni asilimia 11.1 ya wanafunzi wote walioomba mikopo ambao walikuwa 37,315 kwa mwaka 2012/13.
“Hata hivyo, baada ya uchambuzi kwa wanafunzi
37,315 walioomba mikopo hiyo, wanafunzi waliobainika kuwa na sifa ya
kupewa mikopo ni 34,140 lakini waliopata mikopo hiyo ni wanafunzi 30,319
sawa na asilimia 88.9 ya wanafunzi wote waliostahili kupewa mikopo
hiyo,” alisema Mulugo.
Alikuwa akijibu swali la Rashid Ali Abdallah
(Tumbe-Cuf) aliyetaka kujua ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwapatia
mikopo baadhi ya wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo ya elimu ya
juu.
Abdallah pia alihoji Serikali ina mpango gani wa makusudi wa kuhakikisha kuwa wanafunzi waliokosa mikopo hiyo wanapata elimu.
Naibu Waziri alisema, Serikali imetenga kiasi cha
Sh 326 bilioni kwa mwaka 2012/13 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi
95,902 wakiwamo wa mwaka wa kwanza ukilinganisha na Sh 56.1 zilizotengwa
mwaka wa masomo 2005/06.