Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Tume ya Kuchunguza Matokeo Mabaya ya Kidato cha Nne ya mwaka 2012 iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda imemaliza kukusanya maoni ya awamu ya kwanza katika mikoa ya Dodoma, Uguja na Pemba na imeanza awamu ya pili.
Katibu wa Tume hiyo Edwin Mgendela, alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kutoa mawazo yao na kwamba awamu ya kwanza kwenye mji wa Dodoma, Pemba pamoja na Unguja lilimalizika Ijumaa iliyopita.
Alisema katika awamu ya kwanza mkoani Dodoma, Tume ilitembelea Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na baadhi ya halmashauri za mkoa huo na kutembelea shule ilizoelekezwa na katika awamu ya pili iliyoanza jana wajumbe watatembelea vyuo vinavyoandaa walimu kikiwemo Chuo cha Elimu cha Capital, Chuo cha Elimu Mpwapwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
“Kimsingi ziara hiyo inalenga kuangalia na kupata taarifa za namna walimu wanavyoandaliwa, ikiwa ni pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika kuwapika walimu hao pamoja na kupata mtazamo wao,” alisema Mgendela.
Alisema katika awamu ya pili, wajumbe pia watakwenda Dodoma ili kuonana na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, inayoongozwa na Margareth Sitta ili na wao waweze kutoa maoni yao Aprili 11.
Aidha wajumbe wengine watakwenda Zanzibar ili waweze kuonana na Kamati kama hiyo ya Baraza la Wawakilishi, ili na wao watoe maoni yao.
Mgendela alisema kuwa wajumbe wa Tume hiyo kwa siku ya jana, walitarajiwa kuonana na taasisi mbalimbali zinazomiliki shule ili na wao watoe maoni yao.