Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee JKT, Luteni Kanali Martin Mkisi akizungumza kwenye semina hiyo, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu hao.
Alisema ni semina ya kuwajengea uwezo walimu katika ufundishaji kufuatia mtaala mpya ambao unaelekeza mwanafunzi mwenyewe ajieleze uelewa wake kwa kile alichojifunza.
“Semina hii ya siku mbili ni ya kujifunza mbinu mpya za utungaji wa maswali, usahihishaji na ugawaji wa maksi, hivyo ni muhimu sana kwa walimu hasa katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wameonekana kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao,” alisema Mkisi.
Aidha, alisema semina kama hizo zimekuwa zikifanyika ambapo zimekuwa zikitoa fursa kwa walimu kujikumbusha mambo waliyosoma ya ufundishaji.
Mkisi alisema walimu hao ni kutoka Shule ya Sekondari Makongo, Kawawa ya Mafinga mkoani Iringa, Airwing ya Ukonga na Navy Kigamboni Dar es Salaam.
Semina hiyo iliandaliwa na Shule ya Sekondari Jitegemee JKT na kuzishirikisha shule hizo kwa ajili ya kujiongezea uwezo wa ufundishaji