Pages

Welcome to GLOBAL EDUCATION LINK. STUDY ABROAD through US. WE Admit YOU to Overseas Universities, We give YOU right Information, WE Advice on Course Selection, WE Guide YOU On Your CAREER, WE Guide YOU on University SELECTION, WE Assist YOU on YOUR Visa Process. JOIN US NOW OR CALL US ON 0656 200 200 for MORE Information. WELCOME TO FEEL THE DIFFERENCE.

WANAFUNZI 20 WANUSURIKA KIFO


WANAFUNZI zaidi ya 20 wa Shule ya Kimataifa ya St. Charles iliyopo Don Bosco katika Manispaa ya Iringa wamenusurika kifo baada ya gari waliyokuwa wamepanda namba T415 AEG kushindwa kupanda mlima na kupinduka.  

Ajali hiyo ilitokea jana katika eneo la Msikiti wa Hidaya uliopo Kata ya Mvinjeni katikati ya mji wa Iringa. 

Baadhi ya mashuhuda walisema daladala hiyo ilikuwa ikitokea eneo la Frelimo katika Manispaa ya Iringa kwenda mjini Iringa.


Walisema kuwa mara baada ya kufika eneo hilo gari lilishindwa kupanda mlima na kuanza kurudi nyuma kwa kasi kabla ya kupinduka. 

Juma Omari alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, ubovu wa gari pamoja na uzembe wa dereva ambaye alionekana kuendesha gari hilo kwa bila kuchukua tahadhari.

Hata hivyo, alisema kutokana na ajali hiyo dereva na konda waliwatelekeza wanafunzi hao ambao  wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka saba na tisa na kutokomea kusikojulikana na kuwaacha watoto hao bila msaada wowote hadi wananchi walipofika eneo la tukio kuwaokoa.

Wanafunzi hao walichukuliwa na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi. Alisema katika ajali hiyo hakuna aliyepoteza maisha zaidi ya mwanamke mmoja ambaye jina lake halijafahamika kujeruhiwa mikononi. 

Hata hivyo, mmoja kati ya wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji, alisema hali za watoto hao si mbaya bali wamepata michubuko midogo midogo.

Diwani wa Kata ya Mvinjeni, Frank Nyalusi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwapongeza  wananchi wa kata hiyo ambao walifika na kutoa msaada kwa watoto hao kwa kuwakimbiza hospitali.

Wakati huo huo, mwanamke mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja amedaiwa kutaka kuiba mmoja kati ya watoto waliojeruhiwa kwa madai kuwa ni mtoto wake na alikuwa akitaka kumkimbiza Hospitali ya Wilaya ya Iringa badala ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambako majeruhi wengine walikimbizwa.

Mwanamke huyo alishtukiwa baada ya kukutwa akitimua mbio uchochoroni huku akiwa na mtoto. Baada ya kubanwa aliamua kumtelekeza na kukimbia.
Share