Pages

Welcome to GLOBAL EDUCATION LINK. STUDY ABROAD through US. WE Admit YOU to Overseas Universities, We give YOU right Information, WE Advice on Course Selection, WE Guide YOU On Your CAREER, WE Guide YOU on University SELECTION, WE Assist YOU on YOUR Visa Process. JOIN US NOW OR CALL US ON 0656 200 200 for MORE Information. WELCOME TO FEEL THE DIFFERENCE.

WANAFUNZI 4,800 NJOMBE NI MBUMBUMBU

ZAIDI ya wanafunzi 4,800 wa darasa la nne hadi la saba, katika shule za msingi mkoani Njombe hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu. Hayo yalielezwa na Ofisa Elimu Takwimu mkoani hapa, Sandagila Mgaya, alipotoa taarifa ya elimu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na watendaji mbalimbali wa mkoa, Mgaya alisema hali hiyo ni mbaya na inahatarisha maendeleo ya elimu katika mkoa huo mpya.

Alisema kati ya wanafunzi hao wasiojua kusoma, kuhesabu wala kuandika, wapo 19 wanaosoma kidato cha pili na tatu katika shule za sekondari katika mkoa huo.


Utafiti uliofanywa umebainisha kuwa idadi ya wanafunzi hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu imeongezeka jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu katika mkoa huo, alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi alikiri kuwa hali ya elimu mkoani humo ni mbaya na kuwataka wadau wa kikao hicho kujadili uwezekano wa kutatua tatizo hilo.

Alisema lazima kuhakikisha mkoa huo unapata njia ya kuwasaidia wanafunzi hao waweze kusoma, kuandika na kuhesabu ili kukuza kiwango cha elimu mkoani.

“Hali ya elimu ni mbaya kwa matokeo ya kidato cha nne mpaka cha sita, lakini cha ajabu zaidi wapo wanafunzi wengi wa darala la nne hadi la saba, ambao hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu jambo ambalo ni hatari,” alisema.

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Philemon Luhanjo, aliutaka mkoa huo kutilia mkazo elimu ya watu wazima kuwapa elimu ya stadi za maisha wanafunzi wanaomaliza bila kujua kusoma, kuhesabu na kuandika.

Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wadau wa elimu walisema kutojua kusoma, kuandika na kuhesabau kwa wanafunzi hao kunasababishwa na baadhi ya shule kutokuwa na walimu wa kutosha.

Waliitaka Serikali kupunguza idadi ya masomo kwa wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na la pili ili watiliwe mkazo kusoma, kuandika na kuhesabu peke yake.

Suala la kushuka kiwango cha elimu nchini limekuwa gumzo kubwa nchini hivi sasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walishindwa.

Jambo hilo liliibua mjadala mzito katika kikao cha Bunge kilichopita, hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi ambayo pamoja na mambo mengine alitaka iundwe kamati ya bunge kuchunguza mfumo mzima wa elimu nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekwisha kuunda tume inayochunguza kushindwa kwa kiwango kikubwa kiasi hicho kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana.
Share