Makamu wa rais wa
Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo
Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya Saratani.
Rais Chavez alikuwa
anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa
mara ya kwanza tangu maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali
ya kijeshi kuendelea kupokea matibabu. Hata hivyo maelezo zaidi hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu Caracas mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao.
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa.
Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilimali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu masikini.