SERIKALI wilayani Kibondo msako wa kuwasaka watoto wenye umri wa kwenda shule walioko mitaani wakifanya biashara mbalimbali. Mkuu wa Wilaya hiyo, Venance Mwamoto alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kuona kuna wimbi kubwa la watoto wenye umri wa kwenda shule wanaoonekana mjini wakiuza vitu mbalimbali.
Alisema jana waliwakamata watoto 40 wengi wao wakiwa wale walioacha masomo katika vijiji vya wilaya hiyo. Watoto hao wamekimbilia mjini kufanya biashara za kuuza vitumbua, maandazi, kuchunga mbuzi na kufanya kazi za ndani hali inayo mnyima haki motto, alisema. Watoto waliokuwa wamewekwa katika kituo cha polisi, huku wakiwa na ndoo za kuuzia vyakula vya kila aina ni wenye umri kati miaka tisa hadi 16.
Watoto hao waliamuliwa kuacha mizigo yao na kuagizwa kuwafuata wazazi/ walezi ambao ndiyo wanawafanyia kazi na baadaye kuwaamuru warudishwe shule mara moja waendelee na masomo yao. DC alisema mtu yeyote atakayekiuka utaratibu na kumtumikisha mtoto chini ya miaka 18 atafikishwa mahakamani.
Wanafunzi wengi katika Wilaya ya Kibondo wamekuwa wakitoroka masomo na kukimbilia mijini kufanya kazi. Habari zinasema wengi wa watoto hao wamekuwa wakikimbilia Kahama mkoani shinyanga kuchunga ng'ombe na wengine Urambo mkoani Tabora kufanya kazi katika mashamba ya tumbaku.