WANAFUNZI 512 wamefeli mtihani wa kidato cha pili uliofanyika mwaka jana katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, kutokana na ukosefu wa walimu pamoja na utoro kwa wanafunzi. Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Suleiman Liwowa, wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika juzi mjini hapa.
Alisema tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa kuwa nusu ya wanafunzi hao wamefeli na waliofaulu ni 471 kati ya watahiniwa 993.
“Wilaya ya Kilindi haikufanya vizuri matokeo ya kidato cha pili na cha nne na yamesababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa walimu pamoja na mwamko mdogo wa elimu kwa baadhi ya wazazi.
“Hivyo basi, nashauri kikao hiki kitoke na maazimio yatakayoleta matokeo ya haraka kuhusu tatizo hili,” alisema Liwowa.
Katika hilo, alisema wilayani kwake tayari wameshaanza kuchukua hatua ikiwamo kuhamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa vijana wao pamoja na kuongeza idadi ya walimu, ambapo kwa shule za msingi wamepata walimu 135.
“Kwa upande wa shule za sekondari, wizara imetupatia walimu 87 na kwa mwaka huu tumeanza kutoa chakula kwenye shule zote wilayani hapa ili wanafunzi wasipate kisingizio cha kutohudhuria darasani,” alisema Liwowa.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, aliwataka maofisa elimu wote kuhakikisha wanakuja na mipango endelevu itakayoleta matokeo bora ya elimu kwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule zote.
“Naomba niwasisitize kwamba, hakuna asiyeguswa na matokeo haya mabaya na kuna ulazima wa kufanya kazi ya ziada ya kujua namna ya kuwasaidia wanafunzi waliofeli mwaka jana,” alisema Gallawa.
Aliitaka idara ya elimu kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa matatizo ya elimu haraka kabla Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, haijatoa mapendekezo yake kwa nchi juu ya kushuka kwa kiwango cha elimu.